Friday, January 1, 2010

TAIFA LENYE MAONO NA WATU WENYE MAONO


Ukuaji wa Taifa lolote lile duniani unategemea na aina ya maono ya watu au wananchi wanaoishi ndani ya hilo Taifa. Maono ni uwezo wa mtu kuona mambo yajayo kabla ya wengine, kuyaona sana kuliko wengine na kuona mbali zaidi ya wengine.


Ili Taifa likue linahitaji kuwa Taifa lenye maono ya hali ya juu. Na ili maono yawepo panahitajika wawepo watu wachache na sio wote wanaoweza au wenye uwezo wa hali ya juu wa kuona na kubeba maono ya Taifa hilo. Kwa mfano kabla Tanganyika haijapata uhuru palikuwepo na watu wachache wenye uwezo mkubwa wa kuona mbali na kuweza kubeba maono ya Taifa. Watu hawa ndio waliokuwa viongozi na vinara wa kuung’oa utawala Kiingereza katika ardhi ya Watanganyika na kuamua kuunda upya Taifa lao.
 Kimsingi zipo awamu nne tangu Taifa letu lipate uhuru. Katika awamu hizi nne kumekuwepo na matarajio ya kuwa tungekuwa na watu wachache wenye maono ya kulijenga Taifa letu kama ilivyokuwa kwa kipindi cha Mwl. J.K. Nyerere. Mfano mzuri Mwl. Nyerere alikuwa mtu mwenye maono. Mwalimu aliamini katiaka maono yake kwa Taifa na kuwa mstari wa mbele kuongoza Watanzania wenzake. Si kweli kwamba Mwl. Nyerere aliweza kuyafanya mambo yote peke yake la hasha alikuwa na wasidizi wake wa Karibu ambao nao pia waliamini ndani ya maono ya Mwalimu na kuyashika hayo maono. Kwa mantiki hii sasa tunagundua kuwa Mwalimu alikuwa na maono na wasaidizi wake walijifunza ama kuyashika au kuyakataa. Enzi hizo ili Taifa likue ilitegemea ni namna gani wasaidizi wa Mwalimu walikubali kuyashika maono na kuyatendea kazi. Katika kipindi hicho wapo wale walioyashika maono na kuyatendea kazi na wapo baadhi ambao hawakuona umuhimu wa kuyashika maono.

Uwezo wa Taifa kukua unategemea ni namna gani watu wa Taifa hilo wanayashika maono ya kiongozi wao na kuyatendea kazi. Ili Taifa likue linahitaji maono sahihi ya kiongozi wa Taifa. Si kila mtu tunayemwita kiongozi anaweza kubeba maono ndani yake. Na si kila mtu anaweza kubeba maono. Ili kuweka uwiano katikati ya Taifa lazima awepo mtu mmoja ambaye ndani yake anakuwa amebeba “maono ya Taifa lake”. Maono ya Taifa huanza ndani ya mtu mmoja na watu wa Taifa lake huwa watu wenye maono kwa sababu tu wameyashika maono ya mtu mmoja miongoni mwao. Kukikosekana mtu mmoja mwenye maono Taifa hupitia katika vipindi vigumu tofauti na aina ya ugumu unaojitokeza endapo Taifa lina mtu aliyebeba maono na wengine kuyashika. Taifa letu Tanzania linahitaji “maono sahihi” kutoka kwa “mtu sahihi” na Watanzania wote wanahitaji kuyashika maono hayo ili Taifa lao lipige hatua.

Taifa letu Tanzania bado linatembea ndani ya maono ya mtu mmoja ambaye bahati nzuri alishamaliza kazi yake na hivyo maono hayo kufikia ukomo kiuhai. Kuna “maono hai” (active vision) na “maono yaliyokufa” (dormant vision). Tanzania kwa sasa haina “maono hai”. Ni vigumu mtu kuamini kama Tanzana ya sasa haina “maono hai” Lakini ukweli unabakia kuwa Taifa letu kwa sasa halina maono hai. Huhitaji kuwa na elimu kubwa kutambua kuwa Taifa linatembea ndani ya “dormant vision”. Chunguza kasi ya ukuaji wa kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na wa Taifa na kasi ndogo Maendeleo ya jamii utagundua kuwa hatua tulipo sasa ilibidi tuipige zaidi ya miaka 30 iliyopita.Tunaweza kujivunia hatua ile tuliyoipiga sasa, vyema, lakini hatustahili kujivunia kwa sababu Tanzania ni zaidi ya mafanikio yote tuliyonayo sasa. Tanzania haistahili kuwa ilipo sasa. Ipo njia sahihi ya kuifikisha Tanzania inapotakiwa kuwapo. Upo umuhimu wa kila Mtanzania kugundua kuwa hatustahili kuwa hapa tulipo. Tunayo stahili yetu. Na ili kuifikia stahili yetu sharti tukubali kulipia gharama za kuwa na maono hai(active vision). Na huu ndio mwanzo mpya wa maono hai (the new beginning of an active vision).