Tuesday, December 11, 2012

Msingi wa hoja ya Zito katika urejeshwaji wa Mabilioni ya Uswisi na hatua za awali za kichunguzi (Pre-Investigation)

Na Frederick Fussi

Kitabu Kinachoelezea Wezi wa  fedha na Mali
zilizoibiwa na kufichwa nchi za nje
Miezi ya hivi karibuni ndugu Zito Kabwe akiwa kama mbunge na mkereketwa wa masuala ya rushwa aliibua hoja ya ureshwaji ya mabilioni ya Uswisi ambayo taarifa za awali za kichunguzi zinaonesha kuwa mabilioni hayo yalipatikana kwa njia zisizo halali ikiwamo kula rushwa katika upitishwaji wa zabuni serekalini na kuingia mikataba na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Kufahamu jambo hili kwa kina unaweza kurejea hoja binafsi ya Zito Kabwe aliyoiwasilisha bungeni tarehe 8 Novemba 2012 akitaka bunge liunde Kamati maalumu ya uchunguzi ili iweze kubaini nani wanaomiliki mabilioni yaliyofichwa katika mabenki nchini Uswisi na visiwa vingine kama New Jersey na nchi za Uingereza, Ufaransa na kwingineko.

Ikumbukwe kuwa suala la urejeshwaji wa mabilioni ya Uswisi ama kwa Kitaalamu linavyojulikana kama (Asset Recovery) ni jambo geni hapa nchini Tanzania. Hivyo linahitaji mjadala mpana wa kitaalamu ili kusaidia umma wa Watanzania kulifahamu kwa undani na kwa wepesi zaidi.

Msingi wa hoja ya Zito pale bungeni ilikuwa ni kulitumia bunge ambalo ni chombo cha wawakilishi kisheria kulitaka kufanya maamuzi ya kuunda kamati maalumu ya Bunge itakayofanya uchunguzi na na hatimaye Bunge kuielekeza serikali kuchukua hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.

Tunapofikia hatua bunge linatumika na kuombwa kuunda chombo cha kufanya uchunguzi inadhihirishwa kuwa mifumo ya kiserikali ya kufanya uchunguzi dhidi ya rushwa ina dosari, au haiminiki, ama haitimizi majukumu yake, ama haina uwezo (lack of capacity) wa kulifuatilia suala hili ama taasisi hizo zinaingiliwa uhuru wake na serikali ama serikali yenyewe kuwa ujumla imekosa utashi wa kisiasa (Political will) kutaka fedha hizo zirejeshwe. Ukweli huu unatokana na majibu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni baada ya Zito kumaliza kuwasilisha hoja yake. Kufahamu undani wa majibu ya Mwanasheria Mkuu wa serikali fuatilia taarifa za majadiliano ya bunge (Hansard) ya mkutano wa tisa-kikao cha nane kilichofanyika tarehe 8  na 9 Novemba 2012.

Katika sehemu ya majibu ya Mwanasheria Mkuu wa serikali alitoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali kutaka kupata majina ya raia wa Tanzania walioficha fedha nchini Uswisi huku akitumia udhaifu wa sheria ya Uswisi kuonesha kuwa serikali ya Tanzania iliishia hapo na baada ya kuzipatia taarifa hizo alizipeleka kwenye taasisi za ndani za kichunguzi ikiwemo TAKUKURU na Financial Intelligence Unit (FIU) ya Tanzania. Udhaifu wa kisheria uliotumiwa na mwanasheria mkuu wa Serikali ni pale alipokuwa akinukuu sheria ya Uswisi akisemaTukaambiwa mamlaka ile inayofanana na yangu haiwezi kuruhusu uvuaji yaani fishing ya taarifa hizo kwa sababu hilo ni jambo ambalo linahusu nchi nyingine hatuwezi kuwapeleka gerezani”. Aidha inatambulika kuwa majibu kama haya aliyopewa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania pia yamewahi kutolewa kwa nchi nyingine kama Nigeria na Ufilipino ambazo kwa kuwa wao hakujali majibu hayo ya serikali ya Uswisi na waliamua kufanya uchunguzi wa kina kupitia taarifa zao za awali kama hizi zilizoibuliwa na Zito na hatimaye fedha zilizoibiwa zilirejeshwa kwao. Mfano Ufilipino ilifanikiwa kurejesha Dola za kimarekani milioni 684 mwaka 2003 zilizoficha nchini Uswisi na aliyewahi kuwa Rais wa Ufilipino Ndugu Ferdinand Marcos na Nigeria ilifanikiwa kurejesha Dola za Kimarekani milioni 700 ambazo ni sehemu tu ya Dola Bilioni 4 zilizofichwa nje ya nchi na aliyewahi kuwa Rais wa Nigeria, ndugu Sani Abacha.

Sehemu ya hoja ya Zito inatoa taarifa kuwa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 192 ambazo ni sawa na zaidi ya bilioni 314 za Kitanzania ambazo zinasadikiwa kupatikana kwa njia za rushwa zimefichwa na raia wa Tanzania katika mabenki nchini Uswisi.  

Hoja hiyo imesheheni taarifa nyingi za kichunguzi za awali ikiwa ni pamoja na uhusiano kati ya pesa hizo na zabuni zilizowahi kufanywa na serikali kati ya mwaka 2003 na 2008 ambapo inasadikiwa kuwa wanasiasa na watendaji wa serikali “Political Exposed Personalities” walioitumikia serikali katika kipindi hicho walionekana kutunza mabilioni katika akaunti zao nje ya nchi. Uchunguzi wa pesa hizo ndio njia pekee ya kutambua kuwa pesa hizo ni halali ama si halali na baadaye kufanikisha kuzirudisha nchini ili zitumike kwa manufaa ya kijamii.

Urejeshwaji wa fedha haramu na mali za Watanzania zilizopatikana kwa njia za rushwa hauwezi kufanikiwa pasipo kufanyika uchunguzi wa kina ili kubaini Watanzania wenye pesa halali zilizofichwa katika mabenki nje ya nchi na wale wasiokuwa na pesa halali ambazo kimsingi ziliibwa kwa njia ya kupokea rushwa na  wanasiasa na watendaji wa serikali.

Hatua tuliyopo sasa ni hatua za uchunguzi wa awali. Uchunguzi wa awali uliofanywa mpaka sasa haujafanywa na serikali bali umefanywa na watu binafsi (Private Individuals) wenye kuitakia mema Tanzania. Hoja hii ni hoja ya Kitaifa na inapaswa kupewa msukumo wa kitaifa kwa wadau wengine amabao sio sehemu ya serikali (Non state actors).

Non state actors hasa asasi za kirai zinapaswa kuunganisha nguvu ili kufanikisha hatua za awali za kiuchunguzi na hatimaye kuwaelimisha wananchi juu ya sakata hili na kuinyima serikali usingizi kwa kuendelea kuishawishi na kuisukuma serikali kujiingiza katika hatua zinazofuata ili hatua stahiki zichukuliwe na fedha zilizoibiwa(Stollen Assets) zirejeshwe nchini. Kwa kuwa serikali inayosubiri wananchi waipelekee majina ya Watanzania walioficha mabilioni katika mabenki nje ya nchi ni serikali isiyoonesha nia ya dhati ya kupambana na rushwa na ufisadi hivyo inapaswa kuamshwa usingizini na kuendelea kuinyima usingizi kila inapoonesha dalili za kulala tena katika suala hili.

Bunge kwa namna yake limehusika katika sakata hili la urejeshwaji wa hayo mabilioni. Bunge lilitoa maazimio kuwa serikali ilishughulikie suala hilo kwa njia zake. Hivyo bunge limejitoa kabisa katika sakati hili wakati ambapo Serikali haioneshi utashi wa kisiasa katika kufanikisha hatua za awali za kichunguzi ili kusaidia pesa hizo zirejeshwe.  Serikali inafanya hivi kwa kuweka usiri katika shughuli zake za kiuchunguzi lakini imejitega kwa ahadi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa taarifa za uchunguzi huo katika Mkutano wa Kumi na moja.
Ikumbukwe kuwa katika hoja hii Watanzania hawataki tu urejeshwaji wa fedha za Uswisi bali kuna fedha katika nchi nyingine kama Uingereza, Ufaransa, visiwa vya New Jersey, Dubai na kwingineko ambako fedha zinazosadikiwa kupatikana kwa njia za rushwa zimefichwa na raia wa Tanzania wengi wao wakiaminika kuwa wanasiasa waandamizi na watendaji wa Serikali kuanzia mwaka 2003 mpaka 2010. 

Hivyo basi uchunguzi ndio njia pekee ya kufanikisha kubaini na kurejesha mabilioni yote yalioibiwa na viongozi wa Kisiasa na watendaji wa Serikali. Lakini hata hivyo bado tupo katika hatua za uchunguzi wa awali  ambao hufanikishwa na watoa taarifa mbalimbali za masuala ya inteligensia ya fedha (Financial Intelligence) na kujengewa hoja chokonozi na wachambuzi wa masuala kama tunavyofanya hapa. Hatua hii ni muhimu sana hasa katika kujenga uelewa kwa umma na kwa serikali kuwa kuwa jambo hili la mchakato wa kurejesha “Stollen Assets” ni jambo jipya nchini.

Taasisi ya nchini Uswisi, Besel Institute on Governance kupitia kituo chake cha urejeshaji wa fedha zilizoibiwa(International Centre for Asset Recovery) inatoa msaada wa kujenga uwezo na kutoa elimu zaidi juu ya hatua kwa hatua mpaka kufanikisha urejeshaji wa fedha zilizoibiwa. Kwa mujibu wa taasisi hiyo ambayo ina uzoefu na wataalamu waliobobea katika fani ya urejeshaji wa pesa zilizoibiwa inaelezea hatua zaidi za kufuatwa ilikiwa ni pamoja na uchunguzi wa awali (Pre-Investigation), Uchunguzi wenyewe (Investigation), Kupeleka kesi mahakamani ili haki ipatikane(Prosecution) na mwisho urejeshwaji wa fedha zilizoibiwa (Repatriation of stolen Assets).

Hatua tuliyopo sisi hapa nchini petu Tanzania ni hatua ya kwanza kabisa ambayo ni ya uchunguzi wa awali. Uchunguzi huu mara nyingi haufanywi na serikali bali hufanywa na raia wenye kukereketwa na ufisadi, wizi wa mali za umma, dhuluma na wasiopenda utawala wa rushwa. Mpaka sasa hatua hii hatujaifanyia haki kwa kuwa watu binafsi (Individuals) na asasi za kiraia hawajajikita katika kutaka kulifahamu suala hili kwa undani, kulifanyia uchambuzi na uchunguzi vilevile ili kuendelea kujenga hoja zitakazoilazimisha serikali kuingia yenyewe pasipo kutarajia katika hatua ya pili za zote zinazofuata.

Hatua hii ya awali ya uchunguzi inahitaji mshikamano wa kudumu (Sustainable Initiative) ili kuhamia (transition) katika hatua zinazofuata. Hatua hii inahusisha pia kutambua majina ya raia wa Tanzania wenye akaunti zinazotunza mabilioni nje ya nchi. Pia inahusishwa ukusanyaji wa taarifa za fedha za kiintelijensia (intelligence gathering). Ukusanyaji wa taarifa hizi utasaidia waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala kuandika makala na habari za kichunguzi za kutosha na hatimaye kutengeneza chanzo huru cha taarifa (Open source database). Hili likifanikiwa serikali itake isitake italazimika kuingia yenyewe katika hatua zinazofuata pamoja na kuwa inadai kuwa imeshaanza uchunguzi wake.  Katika makala ijayo tutachambua kwa kina hatua zinazofuata.