Nimejikuta napata msukumo mkubwa kutoka ndani yangu kulizungumizia swali hili baada ya tafakuri ya kina kwa muda mrefu takribani mwaka mmoja na zaidi. Katika swali hili napenda kuizungumzia siasa kama mfumo unaotambulika na kukubalika na watu wote katika kuratibu rasilimali zote za taifa, iwe ni watu, fedha, maliasili zote zinazohusika kama maji, ardhi, madini, wanyama pori na misitu katika kumnufaisha mwananchi mmoja mmoja na hatimaye kuleta maendeleo endelevu kwa jamii ya watu wote kama Taifa.
Vile vile katika swali hili ningependa sana walengwa wa kwanza kujiuliza swali hili wawe wananchi wote wa Tanzania lakini hasa ningependa kuwatambua kwa kuwaweka katika makundi yafuatayo:- Kundi la kwanza ni la wananchi wanaojihusisha na siasa katika vyama vya siasa iwe ni chama tawala au vyama vya upinzani. Kundi la pili ni la wananchi wasiojuhisha na vyama vya siasa ila wao hupenda kufuatilia nyendo za kisiasa na kuishia kutoa maoni na mitazamo yao kwa namna mbalimbali. Kundi la tatu ni la wananchi wasiojua nini kinaendelea katika siasa nchini mwao lakini hujikuta wakishiriki katika michakato ya kisiasa bila ya wao kujua, kwa mfano kutakiwa kupiga kura huku akiwa hajui atakayempiga kura ni nani na atafanya nini endapo atachaguliwa kuwa kiongozi ama wa kata, jimbo au Urais.
Siasa kama mfumo nilioulezea hapo juu kwa ufupi huwa na athari chanya au hasi katika maisha ya kila mwananchi wa nchi husika. Kuufahamu mfumo wa kisiasa wa nchi yako ama kutokuufahamu hakuwezi kuzuia uwezo wa mfumo huu kuathiri maisha yako kwa namna zote mbili yaani kwa faida au hasara. Ni vyema kila mwananchi akafahamu kuwa siasa ni maisha yake na maisha yake ni siasa. Hakuna jambo litakalofanyika katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na taifa lisilohusisha utashi wa kisiasa. Hivyo utashi wa kisiasa katika ngazi zote za uongozi wa nchi hauepukiki na kila mwananchi anawajibika kujihusisha na mfumo wa kisiasa ili adhma ya kutumia mfumo wa siasa katika kuratibu rasilimali za taifa umnufaishe yeye binafsi na hatimaye kuleta maendeleo endelevu kwa jamii ya watu wote kama Taifa.
Nchi yetu inajivunia kuwa na historia ya aina yake katika nyanja za kisiasa. Kwa ufupi kabisa nitagusia mtiririko wa kihistoria huku nikitumia maana ya siasa kama “mfumo unaotambulika na kukubalika na watu wote katika kuratibu rasilimali zote za taifa, iwe ni watu, fedha, maliasili zote zinazohusika kama maji, ardhi, madini, wanyama pori na misitu katika kumnufaisha mwananchi mmoja mmoja na hatimaye kuleta maendeleo endelevu kwa jamii ya watu wote kama Taifa”. Kabla ya kupata uhuru wa kisiasa, nchi yetu ilikuwa chini ya mfumo wa kisiasa wa wakoloni ambao wao kama ilivyo desturi ya mfumo wa kisiasa waliutumia kujinufaisha wao na watu wao waliokuwa ughaibuni. Hali tukiwa tunatawaliwa hatukuweza kunufaika na mfumo wa siasa za kikoloni kwa kuwa huo ulilenga kuwanufaisha wananchi wao kwa njia za unyonyaji. Hapo ndipo harakati za kudai “uhuru wa kisiasa” (political liberation) zilipamba moto na hatimaye nchi yetu ikatunukiwa uhuru wa kisiasa Desemba 9 mwaka 1961.
Muelekeo wa kisiasa ukabidilika mara baada ya nchi kupata uhuru wa kisiasa kutoka kuwa na vyama vingi katika utawala wa kikoloni na kuwa na chama kimoja cha siasa katika utawala mpya wa kiafrika. Hapa agenda yetu sisi ikawa ni kuijenga nchi kwa dhana ya kuweka umoja na mshikamano na kuondoa ukabila na udini ulichochewa na wakoloni ili waweze kututawala vizuri. Agenda hii ilikuwa nzuri kwa wakati ule, hasa ukizingatia kuwa wakoloni walitumia kamchezo walichokaita kwa lugha yao kuwa “devide and rule”. Lakini sisi agenda yetu ya kisiasa ilibidi ibadilike ili iweze kukidhi haja ya wananchi wote kunufaika na rasilimali za taifa. Hivyo mfumo wa vyama vingi endapo ungepewa nafasi ungeweza kuongeza kasi ya kutugawanya na hivyo kukosa umoja na mshikamano ambao ungetumika kuijenga nchi yetu ili itunufaishe. Mfumo wa chama kimoja ulikuwa una kasoro zake ambazo kwa wakati huo hazikuwa nyingi ukilinganisha na faida zake, ambazo hadi leo hii matunda yake tunayaona kwa Watanzania wote kuishi kwa upendo, kitu ambacho nchi nyingine zinazotuzunguka hawana.
Dhamira na agenda ya kisiasa wakati wa mfumo wa chama kimoja ulio ongozwa na hayati Baba wa Taifa ulikuwa sahihi kwa wakati wake. Miaka ya 1980 kukatokea msukumo na shinikizo kutoka kwa waliokuwa wakitutawala wakitutaka kurudi kwenye mfumo wa vyama vingi kwa hoja kivuli za kutimiza dhana ya uwajibikaji na kuweka demokrasia, kukatufanya kurudi na kuridhia mfumo ambao wao waliutumia kututawala wakiwa huku kwetu na sasa wangependa kuutumia huku wakitutawala kutokea kwao (ughaibuni). Uamuzi wa kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa uliambatana na mapitio ya katiba ya nchi na sheria zake ili kuzifanya ziweze kukidhi haja ya wakati na kuuratibu mfumo wenyewe, kazi iliyofanywa vyema na tume ya marehemu Jaji Francis Nyalali ambayo ilizitamka sheria takribani 40 kama “bad laws” ambazo zinahitaji mabadiliko ya haraka ili mfumo wa vyama vingi vya siasa uwe na manufaa kwa wananchi wote. Kazi ya kurekebisha au kuzifuta sheria hizi ili zikidhi haja ni hoja ya kisheria sana ambayo huenda naweza nisiitupie macho kwa kina kama ambavyo wangeweza kufanya wanasheria, ila ukweli kuwa chochote katika kufanya mabadiliko ya sheria hizi hakijafanyika sitaacha kuusema ili wanaohusika na kulitatua hili wakumbuke kufanya hivyo pamoja na kuwa ni miaka zaidi ya 15 tangu mapendekezo hayo yatolewe. Kuanzia kwenye hoja hii tunaweza kuanza kuhoji uhalali wa kile tunachosema kupitia vyama vyetu vya siasa kama “agenda” zetu tukianzia na chama tawala ambacho ndicho kilichoishika dola kwa sasa na ndio chama kile kile kilichoishika dola wakati mapendekezo ya tume ya Marehemu Jaji Francis Nyalali yalipotolewa. Wakati huo huo tukijiuliza ni zipi agenda za vyama vya upinzani vyenye ushawishi mkubwa hivi sasa katika vyombo vya maamuzi kama bunge na ambavyo vimeweza kuvumilia kuwa na mfumo wa vyama vingi ndani ya “sheria 40” ambazo zilitamkwa kuwa ni “bad laws” na iliyokuwa tume ya Mheshimiwa Nyalali?. Tunakuja kugundua kuwa agenda “nambari moja” ya kila chama cha siasa ni kushinda uchaguzi mkuu na kuunda dola, jambo lililoshuhudiwa katika miaka 15 iliyopita huku chama tawala kikiibuka na ushindi mkubwa katika viti vya madiwani, ubunge na urais na kuunda dola. Huku vyama vingine vya siasa vinavyotamkwa kuwa vyenye ushawishi mkubwa vikufuatia nyuma na kushika mkia. Baada ya kushindwa kwa “agenda nambari moja” ya kushinda uchaguzi mkuu na kuunda dola kwa vyama vya upinzani tangu mwaka 1995, 2000 na 2005 tumeshuhudia “agenda nambari mbili” ya vyama vya upinzani ya “kuking’oa chama tawala” ikipamba moto huku ikisindikizwa na mbwembwe za kisiasa za kuunda umoja wa vyama vya upinzani agenda iliyoonekana kufeli kutokana na kila chama cha upinzani kuwa na “agenda nambari tatu” inayofanana na “agenda nambari mbili” ya chama tawala ambayo hiyo inalenga kuuendelea kuishika dola kwa udi na uvumba ili kuendela kula keti ya Taifa kama ilivyodhirika kwa wale waliokumbwa na kashfa za ufisadi kama rada, Richmond, ndege ya rais, majengo pacha ya benki kuu na Buzwagi. Agenda nambari mbili ya vyama vya upinzani awali ilionekana kuwa na utashi wenye maslahi ya Kitaifa lakini masikitiko yangu makubwa ni kuwa agenda hii imekumbwa na dhoruba ya “devide and rule” na sasa dhamira ya upinzani kuunganisha nguvu ili kuking’oa chama tawala haitafanikiwa mpaka watakapotambua kuwa “agenda zao” zote haziendani na matakwa ya wananchi wa Tanzania. Matakwa ya wananchi wa Tanzania ni yepi? Tukiligundua hili ni rahisi kwa agenda nambari mbili ya vyama vya upinzani ikafanikiwa na hatimaye kuking’oa chama tawala. Na chama tawala kitajifunza kutoka kwa upinzani juu ya nini wananchi wanataka.
Mimi naona vyama vyetu vya siasa havina agenda sahihi kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Kama agenda ni “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu”(Rapid increase of sustainable development) kwanini ndoa ya vyama vya upinzani ilivunjika? Kama agenda ni “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu” kwa nini zitumike mbinu chafu za kushinda uchaguzi na kuuita ushindi wa kishindo ili muendelee kula keki ya Taifa? Ipo haja ya vyama vya siasa kujipitia upya na kutoa kipaumbele kwa agenda yenye maslahi ya kitaifa ya “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu”. Hii agenda ikitupiwa macho kwa makini itatusaidia.Kama lengo letu likawa moja yaani kuleta kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu, ninayo rai moja tu kwa vyama vya upinzani. Tumeshuhudia vyama vya upinzani vikishindwa vibaya katika chaguzi zilizopita. Mwaka huu(2010) pia kuna uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais na kitu cha kushangaza tayari vyama viwili vya upinzani kati ya vyama vilivyowahi kufunga ndoa huko nyuma kila kimoja kimetangaza nia ya kusimamisha mgombea wake wa Urais katika uchaguzi wa Octoba 2010. Ni uamuzi mzuri tena wa kidemokrasia lakini unatufanya tuendelee kuhoji legitimacy ya agenda za coalition mliyoiunda na iliyofeli. Kama agenda ya vyama vya upinzani ni “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu” nawashauri mvunje vyama vyenu vyote na muunde angalau chama kimoja chenye nguvu kitakachosimamisha mgombea mmoja wa kiti cha urais na mkitumia mwanya huo kuwa na wabunge wengi katika viti vya ubunge ili kupush agenda ya “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu . Katika hili kama agenda zenu zitabakia kuwa zile nilizozitaja hapo juu pindi mnapokuwa kwenye vyama vyenu, napenda nitoe tahadhari kuwa yanaweza kuwafika kama yale yaliyoikumba PNU kule Kenya na baadaye kuleta mvutano wa kugawana madaraka na ODM kama ilivyo kwa ZANU-PF na MDC kule Zimbwabwe, serikali ambazo hazina tija kwa Taifa kwa sababu zinatanguliza maslahi binafsi mbele badala ya maslahi ya Taifa. Ni furaha yangu kuona kuwa kila Mtanzania anayeshiriki katika siasa na atakayepiga kura katika uchuguzi mkuu ujao mwezi Octoba 2010 kwa namna yoyote ile anaipa kipaumbele agenda ya “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu” kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Wakati huo huo kila mmoja hali akitafakari makala hii ajiulize “kwani katika siasa mimi agenda yangu ni ipi?” Ningependa sana agenda yako iwe “kuongeza kasi ya maendeleo na kuyafanya yawe endelevu” kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Mungu wabariki Watanzania wawe na nguvu ya kuliona hili.Mungu Ibariki Tanzania. Mungu Ibariki Afrika, watu wake na viongozi.