Hali ya ukosefu wa fursa za ajira nchini Tanzania inazidi kukua siku hata siku. Hali ambayo inawakumba zaidi vijana ambao wanahodhi asilimia kubwa ya tegemeo katika nguvukazi ya Taifa kwa zaidi ya asilimia 65.
Vijana hawa ambao wanapita katika mifumo ya kuwajenga kitaaluma na fani bado wanakuwa wahanga wakubwa wa kadhia hii ya ukosefu wa fursa za kuajiriwa wala kujiajiri. Hali ambayo ni tete kwani si tu kurudhisha nyuma jitihada za vijana hawa kujiletea maendeleo yao binafsi bali pia kwa kiasi kikubwa inalirudisha nyuma Taifa zima.
Takwimu za ukosefu wa ajira za vijana za asilimia takribani 11 tofauti hata na matarajio ya MKUKUTA ambao ulipanga kushusha ukosefu wa ajira mpaka asilimia 6.9 mnamo mwaka jana, 2010. Licha ya takwimu hizo, bado hazitoi picha ya kutosha ya uhalisia wa hali tete ya ukosefu wa ajira na fursa za uzalishaji pato kwani hali ya sasa na ongezeko la wahitimu toka vyuo vya ufundi na vya elimu ya juu imeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni.
Lakini utete unaweza kudhihirika pia kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa nguvukazi na ajira (ILFS) unaodhihirisha ongezeko la watu takribani 760,000 katika soko la ajira kwa kila mwaka ambapo kati yao ni 40,000 tu ndiyo wanapata ajira kila mwaka ikiacha zaidi ya watu 740,000 bila ajira. Naamini utafiti wa hali ya nguvukazi na ajira (ILFS) ukifanywa mwaka huu ama ujao utatoa majibu yenye kuonyesha hali kuwa mbaya zaidi tofauti na takwimu hizo zilizopatikana mnamo mwaka 2001.
Ni kweli nchi nyingi duniani zinakumbwa na kadhia hii ya ukosefu wa ajira. Lakini kila nchi inavyolishughulikia tatizo hili ndipo utofauti na upekee huonekana. Mathalani vijana wa nchi za Misri, Tunisia hivi karibuni walivyolichukulia tatizo la ukosefu wa ajira na kukithiri kwa hali ngumu katika maisha yao inatoa upekee kwani vijana hao wameweza kumudu kuondosha utawala ambao haukuwa ukionyesha jitihada za kutosha kivitendo kulishughulikia tatizo hilo.
Nchi za ulaya mathalani Ujerumani, zimekuwa pia na tatizo hili lakini jitihada zao za kuhakikisha mafunzo ya kujiajiri na kuweka mifumo ya kitaasisi na kiuwezeshaji kwa vijana hawa inatoa tumaini na upekee wa jinsi nchi inavyojitahidi katika kupambana na hali ngumu ya vijana wanaokosa ajira ama fursa za kujiajiri.
Uwepo wa pensheni kwa wasio na ajira zinazotolewa katika nchi hizo nyingi za ulaya unasaidia kupunguza makali ya maisha kwa vijana wasio na ajira ama pato katika kipindi chao cha mpito mpaka watakapo pata fursa za kushiriki katika uzalishaji mali iwe kwa kuajiriwa ama kujiajiri.
Ukimya wa vijana wa kitanzania haimaanishi wao hawaguswi na utete wa ukosefu wa ajira, lah hasha!
Wala ukimya huu wa vijana nchini Tanzania haimaanishi hawatafakari namna ya wao kujikwamua kutoka katika hali ya ukosefu wa fursa za kuzalisha pato lao. Ukimya huu haumaanishi vijana hawatathmini jitihada za serikali pamoja na wadau katika kusaidia kupunguza makali ya tatizo hili.
Hakika vijana wanaona na wanafikiri. Vijana hawa ambao wengi ni wasomi toka vyuo vya ufundi na elimu ya juu wanauwezo wa kuchambua baina ya kauli tupu zidi ya utendaji wa kauli hizo.
Ikumbukwe si vijana tu katika kuliangalia na kuguswa na athari za ukosefu wa ajira na fursa za uzalishaji wa pato, bali jamii nzima inayowazunguka vijana hawa mathalani wazazi wa vijana ambao wamegharamika katika kuwalea na kuwasomesha vijana hawa wanaumia kila uchao wanapo shuhudia juhudi zao zinagota kwa vijana kukaa majumbani miaka kwa miaka wakisaka ajira ama fursa za kujiajiri.
Najua wapo baadhi ya viongozi au wananchi wanaweza kukimbilia kutoa majibu mepesi katika kadhia hii tete kuwa ni ukosefu wa ari kwa vijana katika kujituma na kujiajiri. Si rahisi kama utamkaji wa matamshi hayo!Kwani hakika hata kwa wenye utashi wa kujiajiri ama hata wale wenye utashi wa kufanya kazi kwa kujitolea wanakubwa na changamoto nyingi sana zinazowakwamisha. (changamoto hizi ni nyingi nitazichambua katika makala zijazo)
Naamini endapo kuna utashi madhubuti wa kulishughulikia tatizo la ukosefu wa ajira na uzalishaji pato kwa vijana njia na mbinu zipo nyingi. Njia na mbinu hizi hazikomei kwa mafunzo ya ujasiliamali kama wengi hukimbilia ama mabadiliko ya kimitaala ya elimu tu bali zapaswa ziende zaidi, mathalani uboreshwaji wa sekta kama sekta za kilimo, utalii, viwanda na biashara ambazo kwa kiasi kikubwa zitazaa matunda ya kupokea vijana wengi zaidi na kusaidia wao kuweza kuzalisha pato lao na kwa Taifa kila uchao.
Ni rahisi sana, unaweza jionea kwa uendeshwaji goi goi wa sekta ya miundo mbinu hususan shirika la ndege la Taifa(ATCL) au shirika la reli (TRL) lilivyo na athari hasi kwa ajira nchini. Endapo mashirika haya mawili yangeweza kuhakikishwa yanaendeshwa kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu yangeweza kuchochea ongezeko kubwa la ajira nchini na kusaidia ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja hususan kwa vijana wetu ambao wanahitimu toka katika vyuo kadha wa kadha nchini na hata wengine toka nje ya nchi.
Ndiyo mantiki ya Hayati Mwl. Nyerere enzi za uongozi wake katika awamu ya kwanza, licha ya jitihada nyingi za kuhakikisha huduma za kijamii mathalani upatikanaji wa elimu kwa ngazi zote tangu awali hadi ile ya watu wazima. Alihakikisha anaimarisha sekta za kilimo na viwanda pasi kusahau miundo mbinu kwa kuimarisha sekta hizi na nyingine kivitendo na si kuishia sera na mipango mitamu mitamu pasi utekelezaji madhubuti.
Naamini endapo kweli tukiwa tunatambua nguvu, tathmani na mchango wa vijana mathalani uliotolewa katika kipindi cha chaguzi zetu nchini kama uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka jana, 2010. Basi viongozi na watumishi wa umma walio madarakani hawana budi kukosa usingizi ama starehe kwa kuhakikisha utatuzi wa kudumu wa ukosefu wa ajira na fursa pana za kujiajiri kwa vijana unafikiwa.
Baruapepe: michaeldalali@yahoo.com
© Michael Dalali, 2011