Na, Frederick Eddie Fussi
Mpaka mwaka 2011 tarehe 31 Desemba Bara la Afrika linakadiriwa kuwa na zaidi ya watumiaji 139 milion wa Mtandao wa internet (wavuti) kati ya raia wake wote bilioni 1 wanaokadiriwa kuishi ndani ya bara hili ambalo ni la pili kwa kuwa na watu wengi duniani likilifuata bara la Asia ambalo linakadiriwa kuwa na watu wapatao bilioni 3.8
Wakati huohuo zaidi ya asilimia 50 ya watu wote wanaoishi barani Afrika wanatajwa kuwa ni vijana na zaidi ya yote nchini Tanzania zaidi ya asilimia 30 ya watu wote ni vijana kati ya umri wa miaka 18 na 35 kundi kubwa ambalo ndani yake kuna watumiaji wengi wa internet na mitandao ya kijamii kwa upana wake.
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na TCRA (Mamlaka ya Kuratibu Mawasiliano Tanzania) zinaonyesha matumizi ya internet hapa Tanzania mpaka mwezi Juni 2010 ni asilimia 99 ya wanakaya/mtu mmoja mmoja wapatao 483,204 ambao hawa wote ndio hujishughulisha na matumizi ya internet. Pamoja na hayo hakuna tafiti zinazojishughulisha kusema hasa matumizi ya internet yameisaidiaje Tanzania katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo mintarifu hili la kuandika Katiba Mpya ya Tanzania. Lakini hapana shaka yapo mabadiliko yanayotokana na matumizi hayo ya internet hapa nchini. Pia tunaweza kukusudia kuitumia internet/mitandao ya kijamii kuandika katiba Mpya ya Tanzania.
Matumizi ya internet hapa nchini yamejikita katika kutuma na kupokea barua pepe hasa katika maofisi makubwa (iwe ni serikalini ama makampuni binafsi) na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Sehemu inyobakia ya watumiaji wa internet ni mahususi kwa ajili ya mawasiliano ya tovuti na blogu ikiwa ni pamoja na matumizi wa mitandao ya kijamii kama Facebook, Skype, Twitter na Youtube.
Matumizi ya mitandao ya kijamii ya Facebook, Skype, Twitter na YouTube siku za hivi karibuni yamekithiri sana miongoni mwa vijana hapa nchini, kati ya mitandao hiyo inayooonekana kupendwa zaidi ama kutumiwa na watu wengi ama kuvutia watumiaji wengi kupashana habari ni mtandao wa Facebook. Twitter inaonekana kuvutia vijana wachache ambao kwa maoni yangu wanaonekana kuwa makini (serious minded people).Leo sitazungumzia twitter sana bali facebook.
Ufundi wa kutumia Facebook na Twitter kuweka ujumbe unatofautiana na hii inaweza ikawa sababu kubwa ya kwanini watumiaji wengi wa Facebook hawapendelei kutumia Twitter. Katika Facebook utatakiwa kuweka ujumbe kwa kadiri ya wingi wa maneno yako lakini hali kwa Twitter ni tofauti sana, utatakiwa kuweka ujumbe mfupi, unaoleweka na unapewa nafasi ndogo kuuwasilisha ujumbe wako kwa umakini wa hali ya juu.
Matumizi ya Skype na YouTube mara nyingi huonekana kutumiwa aidha na watu walioko ng’ambo ya nchi kuwasiliana na ndugu zao na marafiki kwa kupitia mawasiliano ya sauti ama mawasiliano ya video fupi (video clip). Matumizi ya mitandao hii miwili hapa nchini kwa sasa haijashika kasi ukilinganisha na nchi za jirani kama Kenya, Uganda na Afrika ya Kusini.
Sehemu kubwa ya matumizi ya mtandao wa Facebook kwa mfano hayajaonekana kuwa ya kimalengo.(Objective or rational). Matumizi hayo kwa hapa Tanzania ni kama sehemu ya kusalimiana na marafaki, kutaniana na kujenga mahusiano ambayo hata hivyo siyo ya msingi sana.Sehemu kubwa ya mijadala ya facebook kwa sasa ni mizaha tupu!Hali hii inatilia mashaka juu ya aina ya watu Watakoishi Tanzania ya kesho.
Ikiwa hii pekee haitoshi, huenda Watanzania watakuwa wamelala usingizi au ni ujinga wa kutojua namna bora ya kuleta maendeleo na mabadiliko ya haraka kupitia mitandao hii ya kijamii kama ilivyoonekana kwa baadhi ya nchi za Kaskazini mwa Afrika kama Tunisia na Misri.
Mabadiliko na maendeleo ya matumizi ya mitandao hii ya kijamii hasa Facebook inabidi yaanze kuonekana sasa. Nimezungumzia kuwa matumizi ya hivi sasa hayapo objective/rational. Nia yangu nitumie mfano rahisi wa uhitaji wa
Katiba Mpya ya Tanzania na kuelezea namna bora ya matumizi ya Mitandao ya kijamii ambayo ni objective/rational. Na endapo yakieleweka na kutumiwa na vijana wote kwa idadi yao kwa wale wanaotumia Facebook wanaweza kuwahamasisha na idadi ya vijana wasio watumiaji kwa pamoja kuandika katiba mpya kutokea Facebook.
Ieleweke kuwa sheria ya ya Tume ya Kuboresha Katiba Mpya ya Tanzania imeundwa na bunge na kupitishwa na Rais. Bunge linawawakilishi wetu ambao sehemu kubwa ya hao ni Chama Tawala CCM ambao tangu awali hawakuonekana kuunga mkono nia na hoja ya kuwa na Katiba Mpya mpaka waliposhinikizwa na kundi kubwa la wanaharakati nje ya bunge na wale wachache ndani ya bunge wakiongozwa na kambi rasmi ya upinzani bungeni chini ya CHADEMA.
Kupita mitandao ya kijamii hapa nazungumzia Facebook, vijana wanaweza kuubadilisha mchezo, badala ya mjadala na taratibu za kuandikwa kwa katiba Mpya kusimamiwa na sheria ambayo ilizua zengwe katika kujadiliwa kwakwe mpaka kupitishwa kwake na
kutiliwa saini na Mhe. Rais, vijana wanaweza kubadilisha mchezo
kwa kuwa wanatumia muda mwingi Facebook wakaamua kuitumia facebook kujadili mambo wanayotaka/wanayodhani kuwa ni muhimu yawepo ndani ya katiba mpya.
Tume imepewa mamlaka ya kisheria kuandika nakala ya kwanza(first draft) ya Katiba ili ipelekwe katika Constituent Assembly (Bunge Maalumu la Kikatiba) ijadiliwe na baadaye ipitishwe na Wananchi kwa njia ya kura ya maoni(Referendum).
Kimsingi, facebook inaweza kutumiwa na vijana na kuishawishi tume badala ya kutumia mabilioni ya shilingi kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni basi waanze kukusanya maoni kwa njia ya mitandao ya kijamii endapo vijana wenyewe tunaotumia mitandao hii tutakuwa serious (makini). Uwezekano huo ni mkubwa. Kupita mijadala mikali ya facebook tunaweza kuishawishi Tume ya Jaji Warioba kufuatilia na kukusanya maoni yetu, hapana shaka tutaandika historia kwa katiba yetu kuandikwa kutokana na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano(TEHAMA).
Leo hii wanaopata fursa ya kwenda katika mikutano ya Tume kutoa maoni ni wachache sana ukilinganisha na wale wanaoingia Facebook kwa siku moja ambapo Facebook inakadiriwa kuwa na watumiaji 549,900 hapa Tanzania (hii ni kwa mujibu wa takwimu za matumizi ya Facebook Tanzania: http://www.socialbakers.com/facebook-statistics/tanzania).
Asilimia 1.31 ya Watanzania wote hutumia Facebook, kati ya hao takribani asilimia 81.35 ya watumiaji wote hao wanaitumia facebook kwa wingi zaidi. Hii wataalamu hiita (Penetration of online Popuation). Hii maana yake ni kuwa hiyo asilimia 1.31 ya watumiaji wote wa facebook hapa Tanzania wanatumia muda wao mwingi sana wakiwa ndani ya mtandao huu wa facebook. Hawa ni watu wanaojua kusoma na kuandika, wanaouwezo mzuri wa kufikiria ila ni wavivu kutambua fursa ya kuitumia facebook kushinikiza mabadiliko na mabadiliko hapa nazungumzia kaundika katiba mpya kupitia Facebook.
Sasa, shinikizo la mabadiliko ya Watanzania kupita facebook ndio pengine njia pekee ya kuisaidia Tume ya Jaji Warioba na pengine kuubadilisha mchezo wa Tume badala ya wao kuwafuata wananchi kule walipo na kuishia kuwasilikiza wananchi wasiozidi 100 kwa siku kwa nini wasije Facebook kuwasilikilza zaidi ya Watanzania laki 5 wanaotaka katiba yao iweje? Mpaka.
Rai yangu kwa leo ni kuwa tunaweza kuandika Katiba Mpya kupitia Facebook endapo tukaongeza umakini na kupanua mawazo yetu katika matumizi yetu ya facebook kwa siku. Wajanjwa wachache wamefanya mbinu za kutengeza utaratibu wa Tume kukusanya maoni wakijua kuwa sisi ni wavivu kupanga foloni za kusubiria kuongea wakati tume ikija, wakati mwingine mijadala yenyewe inakuwa boring, lakini tukitumia facebook ama mitandao mingine ya kijamii hatuhitaji kupanga foleni ya kusubiri kuongea mbele ya makamishna wa tume!
Mkakati wa sasa wa tume ya Jaji Warioba, pamoja na kuwa utaonekana ndio njia muafaka ya kuanza mchakato wa kuandika katiba Mpya bado vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa Mitandao ya Kijamii tunaweza kuitumia kubadilisha historia ya nchi yetu.
Katika toleo lijalo nitaelezea njia madhubuti za kutumia Facebook na mitandao mingine ya kijamii kuandika Katiba Mpya badala ya kutegemea Tume ya jaji Warioba ambayo kimsingi haina uwezo wa kufikia kila mwananchi ili atoe maoni yake. Ni rahisi kufanya ushawishi kutumia nyenzo hii.
Kwa sasa unaweza kutembelea blogu ya Asasi ya TYVA ambayo inaendesha mradi uitwao IJUE KATIBA, hapa http://ijuekatiba.wordpress.com/harakati-mtandaoni/ Vilevile unaweza kutembelea Ukuarasa wa IJUE KATIBA uliopo Facebook kupitia anuani hii: http://www.facebook.com/groups/214223971930520/
Katiba Mpya lazima tuiandike wenyewe, tumenyanyasika vya kutosha, tumenyonywa vya kutoshwa, sasa ni wakati wa mabadiliko ya kweli. Harakati ziendelee na njia pekee ya kuleta mabadiliko ni kutumia mtaji wetu wa akili ndani ya kundi kubwa la vijana wa sasa hapa kwetu Tanzania.
Frederick Fussi, ni mwanaharakati katika shirika la Vijana Tanzania Youth Vision Association(TYVA).