Na Frederick Fussi
Kitabu Kinachoelezea Wezi wa fedha na Mali zilizoibiwa na kufichwa nchi za nje |
Kufahamu jambo hili kwa kina unaweza kurejea hoja binafsi ya
Zito Kabwe aliyoiwasilisha bungeni tarehe 8 Novemba 2012 akitaka bunge liunde
Kamati maalumu ya uchunguzi ili iweze kubaini nani wanaomiliki mabilioni
yaliyofichwa katika mabenki nchini Uswisi na visiwa vingine kama New Jersey na
nchi za Uingereza, Ufaransa na kwingineko.
Ikumbukwe kuwa suala la urejeshwaji wa mabilioni ya Uswisi
ama kwa Kitaalamu linavyojulikana kama (Asset Recovery) ni jambo geni hapa
nchini Tanzania. Hivyo linahitaji mjadala mpana wa kitaalamu ili kusaidia umma
wa Watanzania kulifahamu kwa undani na kwa wepesi zaidi.
Msingi wa hoja ya Zito pale bungeni ilikuwa ni kulitumia
bunge ambalo ni chombo cha wawakilishi kisheria kulitaka kufanya maamuzi ya
kuunda kamati maalumu ya Bunge itakayofanya uchunguzi na na hatimaye Bunge
kuielekeza serikali kuchukua hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha
na mali haramu nje ya nchi.
Tunapofikia hatua bunge linatumika na kuombwa kuunda chombo
cha kufanya uchunguzi inadhihirishwa kuwa mifumo ya kiserikali ya kufanya
uchunguzi dhidi ya rushwa ina dosari, au haiminiki, ama haitimizi majukumu
yake, ama haina uwezo (lack of capacity) wa kulifuatilia suala hili ama taasisi
hizo zinaingiliwa uhuru wake na serikali ama serikali yenyewe kuwa ujumla
imekosa utashi wa kisiasa (Political will) kutaka fedha hizo zirejeshwe. Ukweli
huu unatokana na majibu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni baada ya Zito
kumaliza kuwasilisha hoja yake. Kufahamu undani wa majibu ya Mwanasheria Mkuu
wa serikali fuatilia taarifa za majadiliano ya bunge (Hansard) ya mkutano wa
tisa-kikao cha nane kilichofanyika tarehe 8 na 9 Novemba 2012.
Katika sehemu ya majibu ya Mwanasheria Mkuu wa serikali
alitoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali kutaka kupata majina ya
raia wa Tanzania walioficha fedha nchini Uswisi huku akitumia udhaifu wa sheria
ya Uswisi kuonesha kuwa serikali ya Tanzania iliishia hapo na baada ya
kuzipatia taarifa hizo alizipeleka kwenye taasisi za ndani za kichunguzi
ikiwemo TAKUKURU na Financial Intelligence Unit (FIU) ya Tanzania. Udhaifu wa
kisheria uliotumiwa na mwanasheria mkuu wa Serikali ni pale alipokuwa akinukuu
sheria ya Uswisi akisema “Tukaambiwa
mamlaka ile inayofanana na yangu haiwezi kuruhusu uvuaji yaani fishing
ya taarifa hizo kwa sababu hilo ni jambo ambalo linahusu nchi nyingine hatuwezi kuwapeleka gerezani”. Aidha inatambulika kuwa majibu kama
haya aliyopewa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania pia yamewahi kutolewa
kwa nchi nyingine kama Nigeria na Ufilipino ambazo kwa kuwa wao hakujali majibu
hayo ya serikali ya Uswisi na waliamua kufanya uchunguzi wa kina kupitia taarifa
zao za awali kama hizi zilizoibuliwa na Zito na hatimaye fedha zilizoibiwa
zilirejeshwa kwao. Mfano Ufilipino ilifanikiwa kurejesha Dola za kimarekani milioni
684 mwaka 2003 zilizoficha nchini Uswisi na aliyewahi kuwa Rais wa Ufilipino
Ndugu Ferdinand Marcos na Nigeria ilifanikiwa kurejesha Dola za Kimarekani
milioni 700 ambazo ni sehemu tu ya Dola Bilioni 4 zilizofichwa nje ya nchi na
aliyewahi kuwa Rais wa Nigeria, ndugu Sani Abacha.
Sehemu ya hoja ya Zito inatoa taarifa kuwa jumla ya Dola za
Kimarekani Milioni 192 ambazo ni sawa na zaidi ya bilioni 314 za Kitanzania
ambazo zinasadikiwa kupatikana kwa njia za rushwa zimefichwa na raia wa
Tanzania katika mabenki nchini Uswisi.
Hoja hiyo imesheheni taarifa nyingi za kichunguzi za awali
ikiwa ni pamoja na uhusiano kati ya pesa hizo na zabuni zilizowahi kufanywa na
serikali kati ya mwaka 2003 na 2008 ambapo inasadikiwa kuwa wanasiasa na
watendaji wa serikali “Political Exposed Personalities” walioitumikia serikali
katika kipindi hicho walionekana kutunza mabilioni katika akaunti zao nje ya
nchi. Uchunguzi wa pesa hizo ndio njia pekee ya kutambua kuwa pesa hizo ni halali
ama si halali na baadaye kufanikisha kuzirudisha nchini ili zitumike kwa
manufaa ya kijamii.
Urejeshwaji wa fedha haramu na mali za Watanzania
zilizopatikana kwa njia za rushwa hauwezi kufanikiwa pasipo kufanyika uchunguzi
wa kina ili kubaini Watanzania wenye pesa halali zilizofichwa katika mabenki nje
ya nchi na wale wasiokuwa na pesa halali ambazo kimsingi ziliibwa kwa njia ya
kupokea rushwa na wanasiasa na watendaji
wa serikali.
Hatua tuliyopo sasa ni hatua za uchunguzi wa awali. Uchunguzi
wa awali uliofanywa mpaka sasa haujafanywa na serikali bali umefanywa na watu
binafsi (Private Individuals) wenye kuitakia mema Tanzania. Hoja hii ni hoja ya
Kitaifa na inapaswa kupewa msukumo wa kitaifa kwa wadau wengine amabao sio
sehemu ya serikali (Non state actors).
Non state actors hasa asasi za kirai zinapaswa kuunganisha
nguvu ili kufanikisha hatua za awali za kiuchunguzi na hatimaye kuwaelimisha
wananchi juu ya sakata hili na kuinyima serikali usingizi kwa kuendelea
kuishawishi na kuisukuma serikali kujiingiza katika hatua zinazofuata ili hatua
stahiki zichukuliwe na fedha zilizoibiwa(Stollen Assets) zirejeshwe nchini. Kwa
kuwa serikali inayosubiri wananchi waipelekee majina ya Watanzania walioficha
mabilioni katika mabenki nje ya nchi ni serikali isiyoonesha nia ya dhati ya
kupambana na rushwa na ufisadi hivyo inapaswa kuamshwa usingizini na kuendelea
kuinyima usingizi kila inapoonesha dalili za kulala tena katika suala hili.
Bunge kwa namna yake limehusika katika sakata hili la
urejeshwaji wa hayo mabilioni. Bunge lilitoa maazimio kuwa serikali ilishughulikie
suala hilo kwa njia zake. Hivyo bunge limejitoa kabisa katika sakati hili
wakati ambapo Serikali haioneshi utashi wa kisiasa katika kufanikisha hatua za
awali za kichunguzi ili kusaidia pesa hizo zirejeshwe. Serikali inafanya hivi kwa kuweka usiri katika
shughuli zake za kiuchunguzi lakini imejitega kwa ahadi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kutoa taarifa za uchunguzi huo katika Mkutano wa Kumi na moja.
Ikumbukwe kuwa katika hoja hii Watanzania hawataki tu
urejeshwaji wa fedha za Uswisi bali kuna fedha katika nchi nyingine kama
Uingereza, Ufaransa, visiwa vya New Jersey, Dubai na kwingineko ambako fedha
zinazosadikiwa kupatikana kwa njia za rushwa zimefichwa na raia wa Tanzania
wengi wao wakiaminika kuwa wanasiasa waandamizi na watendaji wa Serikali
kuanzia mwaka 2003 mpaka 2010.
Hivyo basi uchunguzi ndio njia pekee ya kufanikisha kubaini
na kurejesha mabilioni yote yalioibiwa na viongozi wa Kisiasa na watendaji wa
Serikali. Lakini hata hivyo bado tupo katika hatua za uchunguzi wa awali ambao hufanikishwa na watoa taarifa
mbalimbali za masuala ya inteligensia ya fedha (Financial Intelligence) na kujengewa
hoja chokonozi na wachambuzi wa masuala kama tunavyofanya hapa. Hatua hii ni
muhimu sana hasa katika kujenga uelewa kwa umma na kwa serikali kuwa kuwa jambo
hili la mchakato wa kurejesha “Stollen Assets” ni jambo jipya nchini.
Taasisi ya nchini Uswisi, Besel Institute on Governance
kupitia kituo chake cha urejeshaji wa fedha zilizoibiwa(International Centre
for Asset Recovery) inatoa msaada wa kujenga uwezo na kutoa elimu zaidi juu ya
hatua kwa hatua mpaka kufanikisha urejeshaji wa fedha zilizoibiwa. Kwa mujibu
wa taasisi hiyo ambayo ina uzoefu na wataalamu waliobobea katika fani ya
urejeshaji wa pesa zilizoibiwa inaelezea hatua zaidi za kufuatwa ilikiwa ni
pamoja na uchunguzi wa awali (Pre-Investigation), Uchunguzi wenyewe
(Investigation), Kupeleka kesi mahakamani ili haki ipatikane(Prosecution) na
mwisho urejeshwaji wa fedha zilizoibiwa (Repatriation of stolen Assets).
Hatua tuliyopo sisi hapa nchini petu Tanzania ni hatua ya
kwanza kabisa ambayo ni ya uchunguzi wa awali. Uchunguzi huu mara nyingi
haufanywi na serikali bali hufanywa na raia wenye kukereketwa na ufisadi, wizi
wa mali za umma, dhuluma na wasiopenda utawala wa rushwa. Mpaka sasa hatua hii
hatujaifanyia haki kwa kuwa watu binafsi (Individuals) na asasi za kiraia hawajajikita
katika kutaka kulifahamu suala hili kwa undani, kulifanyia uchambuzi na
uchunguzi vilevile ili kuendelea kujenga hoja zitakazoilazimisha serikali
kuingia yenyewe pasipo kutarajia katika hatua ya pili za zote zinazofuata.
Hatua hii ya awali ya uchunguzi inahitaji mshikamano wa
kudumu (Sustainable Initiative) ili kuhamia (transition) katika hatua
zinazofuata. Hatua hii inahusisha pia kutambua majina ya raia wa Tanzania wenye
akaunti zinazotunza mabilioni nje ya nchi. Pia inahusishwa ukusanyaji wa
taarifa za fedha za kiintelijensia (intelligence gathering). Ukusanyaji wa
taarifa hizi utasaidia waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala kuandika
makala na habari za kichunguzi za kutosha na hatimaye kutengeneza chanzo huru
cha taarifa (Open source database). Hili likifanikiwa serikali itake isitake
italazimika kuingia yenyewe katika hatua zinazofuata pamoja na kuwa inadai kuwa
imeshaanza uchunguzi wake. Katika makala
ijayo tutachambua kwa kina hatua zinazofuata.