Tuesday, February 16, 2010

UONGOZI NI MAONO

Sifa ya Kiongozi yeyote yule duniani katika nyanja za kila namna ni sharti awe amebeba maono ndani yake ili aweze kuongoza au kuliongoza kundi kwa usahihi mkubwa. Labda tujiulize kwa nini kundi linahitaji kuongozwa?

Hakuna dereva anayeweza kuendesha gari vizuri asipoifahamu barabara aiendeayo au kuufahamu mwisho wa safari yake. Kadhalika kiongozi naye ni lazima afahamu watu anaowaongoza na kutambua kule anakowapeleka. Tunamfananisha kiongozi mzuri na dereva stadi anayelifahamu gari lake kwa ufasaha na kuweza kulichunguza kwa makini na kabla ya hayaanza safari yake hujenga picha akilini mwake juu ya kule anakotakiwa kulifikisha gari lake kwa usalama wa hali ya juu. Dereva huyu lazima kwa namna moja ama nyingine atakuwa amepakia abiria au mizigo ndani ya gari lake. Uwezo wa dereva kupiga picha ya safari nzima tungu mwanzo wa safari hadi mwisho wake humfanya dereva kuwa na sifa ya maono. Hatumtegemei dereva huyo kufanya tofauti na maono yake. Maono yake ni kuliendesha gari lake kupitia barabara fulani kwa mwendo fulani na kufika sehemu husika ndani ya muda uliopigiwa mahesabu. Kuzifahamu changamoto zitakazomkabili njiani wakati wa safari nayo pia ni sifa ya dereva huyu mzuri mwenye maono.

Kadhalika kwake kiongozi mwenye maono huwafahamu watu wake vizuri, huzijua changamoto za watu wake na yeye hufahamu namna bora ya kuzikabili hizo changamoto ili aweze kulipigisha hatua kundi lake. Kiongozi bora ni mwenye maono mithili ya mchungaji wa kondoo. Mchungaji wa kondoo huwatoa zizini asubuhi hali akifahamu aina ya malisho sahihi kwa ajili ya afya ya kondoo wake. Hufamu vyema mto ule wenye maji safi na salama ambayo kondoo wake watayanywa wakiwa malishoni. Wanyang’anyi wajaposogelea kundi la kondoo wake yeye husimama kidete kuwatetea kwa kuwa ana maono ya kuwarudisha salama katika zizi lile lile alilowatoa asubuhi.

Uongozi ni maono, pasipo maono uongozi huwa mgumu na mafanikio habakia kuwa ndoto miongoni mwa kundi ama watu wanaoongozwa. Kiongozi hubeba maono ambayo hushikwa na wale anaowaongoza. Uwezo wa kundi kuyashika maono ya kiongozi wao ndio uwezo wa kundi kufanikiwa na kuwa salama nyakati zote. Wapo watu ambao sio viongozi lakini wanaongoza. Watu wa namna hii hutawaliwa na nyakati zisizokuwa na mafanikio yaliyo dhahiri. Viongozi hawa huwa na sifa ya kukosa maono na uzoefu anonesha kuwa viongozi hawa huliyumbisha kundi wanaloliongoza. Uongozi ni maono, maono hayo hubaki kuwa msaada mkubwa kwa kuwa watu au kundi linaloongozwa na kiongozi mwenye maono hufanikiwa kwa kasi ya ajabu kwa sababu imo siri kubwa ndani ya kiongozi aliyebeba maono sahihi na maono hayo yakashikwa na kundi lake.