Wednesday, July 31, 2013

Uwezo wa kiongozi kuwafahamu watu wake ndio uwezo wa uongozi wake

Na Frederick Fussi. Dar es Salaam. 31 Julai 2013.Mbezi beach

Mnamo tarehe 24 Julai mpaka 26 Julai mwaka huu (2013) nilikuwa na vijana wenzangu kadhaa katika mafunzo ya Uongozi kwa Vijana (Young Leaders Training Programme).

Mafunzo haya yanayoandaliwa kila mwaka na Taasisi ya Kisiasa ya nchini Ujerumani ijulikanayo kama Friedrich Ebert Stiftung (FES)  yalifanyika katika kituo cha Mikutano Kibaha (Kibaha Conference Center)

Viongozi wengi hapa Tanzania wamewahi kupata mafunzo ya namna hii ya uongozi kutoka FES ambapo mafunzo hufanyika katika muktadha wa nchi husika na kuongozwa na muwezeshaji wa ndani ya nchi, mwenye uzoefu na aliyebobea katika masuala ya uongozi.

Moja kati ya mambo tuliyokuwa tukijifunza katika mafunzo haya ni sifa za uongozi ama unaweza kuziita sifa za kiongozi. Tulitaja sifa nyingi na kuzijadili ikiwa ni pamoja na uadilifu, kuwa mfano wa kuigwa, kuwa mwenye maarifa, kuwajibika, muwazi, kuwa na dira (visionary), ubunifu na sifa nyinginezo ambazo safu hii isingetosha kuzitaja.

Pamoja na sifa zote tulizojadili nimegundua kuwa  tulisahau kutaja sifa moja ambayo ni muhimu kiongozi akawa nayo. Sifa hii ni ile  ya uwezo wa kiongozi kuwafahamu watu wake.

Miaka ya hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa maarifa, taarifa na utandawazi sifa hii ya kiongozi kuwafahamu watu wake imeanza kutoweka miongoni mwa viongozi.

Kiongozi anaweza akatumia uwezo wake wa fedha akampatia kazi mtaalamu (Consultant) amsaidie kufanya uchambuzi wa masuala yahusuyo watu, lakini sio kwa kiongozi huyo kujibiidiisha kuwafahamu watu wake kwa undani.

Kuna tofauti kati ya kiongozi kuzungumzia masuala (issues) zinazowakabili watu na kiongozi kuwafahamu watu wake. Hapa sizungumzii ufahamu wa masuala bali nazungumzia sifa ya kuwajua watu wako kwa undani, kujua wanalaa katika nyumba ya aina gani, wanakula nini, shughuli zao ni zipi, kipato chao kipoje wanavaa nini na endapo wana usalama kwa kiwango gani.

Uelewa wa masuala (issue) unaotokana na rejea za vitabu, ripoti mbalimbali na wakati mwingine vyombo vya habari, huu huwa ni uelewa wa jumla jumla. Kiongozi anaweza kuchukua masuala ya jumla kisha akazungumzia athari za masuala hayo na baadhi ya wananchi wakampenda kwa umahiri wake wa kuelezea shida zao na suluhu za shida zao, akaishia hapo.
Wiki chache zilizopita tukiwa katika mafunzo haya haya ya uongozi tumekuwa tukizungumzia kwa jumla jumla juu ya tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini. Tulifanya rejea katika mada iliyowasilishwa na Dr. George Nangale chini ya kichwa cha habari “Nafasi ya nchi katika maendeleo ya uchumi: Changamoto za ajira Afrika Mashariki-mfano wa Tanzania”. Mada hii iliwasilishwa kwa mara ya kwanza tarehe 24-25 Septemba 2012 nchini Kenya, Nairobi katika mkutano wa sera za ajira za nchi washirika wa Afrika mashariki.

Rejea nyingine tulizofanya ni sera ya Taifa ya Ajira (2008) na rejea binafsi ambazo mimi nilifanya ni pamoja na Integrated Labour Force Survey, (2006). Uchambuzi wangu na mchango wangu katika mjadala ulilenga hasa katika tafsiri ya ajira kwa mujibu wa sera ya Taifa ya ajira.
Mchango wangu ukaegemea katika muktadha wa namna vijana wa hapa nchini wanaweza kujenga fursa za ajira katika kilimo. Msingi wa hoja yangu ulijengwa katika maana tatu za tafsiri ya ajira kwa mujibu wa sera ya Taifa ya ajira.

Sera hii inatambua ajira inakamilika yakiwapo mambo matatu, mosi ajira ni sharti iwe ni shughuli ya kisheria, pili iwe shughuli yenye staha na tatu iwe shughuli yenye kutengeneza kipato.

Nchini kwetu zipo sekta sita za ajira ikiwamo Serikali, mashirika ya umma, sekta binafsi, sekta isiyo rasmi, sekta ya kilimo na sekta ya kaya (household sector). Niling’amua kuwa sekta ya kilimo inaongoza kwa kutotimiza sharti la mwisho la tafsiri ya ajira, kama ilivyoelezewa na dira ya sera ya Taifa ya ajira (2008).

Sekta ya kilimo inaunda asilimia 74 ya watu 16milioni walioajiriwa nchini ambapo asilimia 0.0 pekee ndio hutengeneza kipato kutokana na kushughulika moja kwa moja katika kilimo.

Hoja yangu ikawa kuwa kwa kuwa kilimo kinaajiri sehemu kubwa ya watu waliokuwa katika ajira nchini kuna haja ya kuwepo mabadiliko ya kisera yatakayowezesha kilimo kitimize masharti yote matatu ya ajira (shughuli ya kisheria, yenye staha na inayozalisha kipato kwa wingi).

Tukiishia katika mabishano ya hoja katika mafunzo yetu ya viongozi, huenda hoja yangu ikawa na nguvu na ikawa ya maana. Ila udhaifu wa hoja hii ni kuwa hoja inajengwa na rejea ambazo zimelazimisha hoja kuwa ya jumla jumla na mabishano ya hoja baina yangu na viongozi wenzangu yasitoke nje ya mafunzo yetu ya uongozi.

Kama kiongozi nimeishia kujadili hoja jumla jumla, kiwango cha ufahamu wangu kitaishia katika ujumla jumla wa hoja endapo sitakuwa na juhudi za kufanya hoja yangu iwe ya reja reja (specific issue). Mfano nitakaotoa hapo chini kuhusu kijana Hussein mchuuzi wa korosho utatosha kuelezea namna ambavyo hoja yangu ilipaswa kuwa ya reja reja (specific issue) na pia ufahamu kuongezeka kwa kumfahamu kijana huyu aliyekatika ajira isiyorasmi (moja kati ya sekta sita za ajira hapa nchini).

Sasa uwezo wa kujenga hoja kwa namna ya reja reja inahitaji hiki ninachokiita “uwezo wa kiongozi kuwafahamu watu wake”.  Kila kiongozi katika eneo lake la uongozi analojukumu la kufahamu kwa undani watu wake, tabia zao na mienendo yao na endapo mienendo hiyo inausaidia uongozi kufanikisha dhima yake.

Jioni ya leo (31 Julai 2012) nilipokuwa nikirejea toka safari ya kikazi mjini Morogoro kuja jijini Dar es Salaam nilibahatika kukutana na kijana Hussein mchuuzi wa korosho. Korosho ni zao la kilimo hapa nchini  na pia Tanzania ni ya tatu duniani kwa kuzalisha korosho, na ya pili Afrika, wakati mauzo ya nje (export) hufanyika sana nchini India.

Kijana huyu Hussein alipanda ndani ya basi dogo aina ya coster maeneo ya mbezi Louis mkononi akiwa amebeba vifuko vidogo vidogo vya korosho. Kijana huyu alikuja moja kwa moja kuketi pembezoni mwa kiti nilipoketi mimi. Nikaguswa moyoni mwangu kumsemesha na baadaye tukaanza kuongelea biashara yake ndogo ya uchuuzi wa korosho.

Mimi nilidhani kuwa kijana huyo anarejea nyumbani kwake baada ya shughuli zake kumbe ndio kwanza alikuwa anaanza shughuli yake ya uchuuzi wa korosho. Akanieleza kuwa wauza korosho wote mabarabarani wanavikundi vyao, na pia hupata mikopo kutokana na kuwepo katika vikundi hivyo.

Kwa siku Hussein huuza mifuko angalau 20 kila mmoja wenye thamani ya shilingi 1,000.  Wakati mwingine huuza mifuko yenye korosho za thamani ya shilingi 500, 2,000 na 5,000.
Soko hutegemea mitaa atakayozunguka siku hiyo na idadi ya wateja atakaokutana nao. Pia soko hutegemea idadi ya mifuko ambayo yeye mwenyewe huiandaa kila siku. Kazi hii ni nzuri isipokuwa humlazimisha muuzaji kutembea umbali mrefu akitafuta angalau shilingi 20,000 kwa siku.  

Hussein anapata kipato, shuguli yake huenda haivunji baadhi ya sheria, lakini natilia shaka endapo kazi hii ni ya staha kwa kuwa kijana huyu hutembea umbali mrefu hasa nyakati za jioni na usiku jambo ambalo ni hatari kwa usalama wake. Naye alikiri kuwa sio salama sana kutembea usiku.  

Jambo lililoushangaza moyo wangu ni pale kijana huyo aliponieleza kuwa kwa biashara hiyo ya uchuuzi aliyoanza tangu mwaka 2000 ameweza kujenga nyumba ya vyumba vitano huko maeneo ya visiga Kibaha.

Kipindi nakutana na huyu kijana alikuwa amepanga kushuka kituo cha Kona Kimara kisha kuanza kutembeza vifuko vya korosho kuanzia kituo hicho mpaka mbezi mwisho. Akanieleza kuwa wakati mwingine huanzia mwenge, ubungo na kuendelea kutembea mpaka mbezi mwisho ambapo hupanda basi na kurejea kwake Visiga, Kibaha.

Eneo ambalo kijana huyu hufanyia shughuli yake ni jimbo la ubungo na wilaya ya kinondoni ambapo kuna Mbunge na mkuu wa wilaya na madiwani. Eneo ambalo kijana huyo anaishi ni Kibaha ambapo pia ni wilaya na jimbo. Visiga ambapo ndiko yalipo makazi yake pia kuna viongozi wa serikali za kata na mtaa pia.

Maswali baada ya kukutana na kijana huyo yakawa ni kiwango gani viongozi wa maeneo yote niliyotaja hapo juu wanawafahamu watu wao. Mfano huyu kijana anawakilisha wachuuzi wa vitu vya barabarani (sekta isiyo rasmi), kuna vijana wanaojihusisha na biashara ndogondogo kama mama ntilie, kuchoma chipsi, wauza matunda, wanafuzi, waalimu, na wengineo katika makundi mengine. Je mfano mwenyekiti wa serikali za mtaa na wajumbe wake wanafamu idadi ya vijana mtaani kwao wenye kufanya shughuli kama hizo?

Ni kwa kiwango gani kiongozi anawajibika kushuka ngazi ya chini na kujua endapo watu anaowaongoza, mathalani wanafunzi, wanakumbwa na adha zipi katika kufanikisha masomo yao. Waalimu, je wanafanikishaje wajibu wao wa kujenga taaluma katika eneo lako.

Ni kwa kiwango gani viongozi wanaachilia mbali kurejea ripoti za vitabu na rejea mbali mbali na kutenga muda wa kushuka chini kuwafahamu watu wao kwa undani? Kiwango cha kiongozi kufahamu watu wake ndio kiwango chake cha uongozi aliokuwa nao.

Ukiwa kiongozi ukaishia kufahamu mambo yaliyomo vitabuni pekee na kwenye ripoti pekee unawezaje kufanya uhakiki (reconcile) wa ripoti hizo kama sio juhudi binafsi kuwafamu wako wako na kujua endapo ripoti hizo zinawasilisha hali halisi?

Hasara ya kuishia katika rejea za vitabuni, na ripoti nyingine kuhusu maisha ya raia wa eneo husika inaweza kujenga utamaduni wa kuweka mipango na sera kulingana na ripoti hizo jambo linaweza lisiwe na tija endapo hali halisi ni tofauti. Na matokeo (results) au mafanikio ya mipango hiyo ama yawe kidogo sana ama yasiwepo kabisa.  

Hasara nyingine itokanayo na rejea za vitabuni na ripoti za wataalamu ni ubunifu wa sera ambazo hazijawahi kujaribiwa kabla ya kutekelezwa kwa kuwa viongozi hawapati nafasi binafsi ya kuwafahamu watu wao. Simaanishi kuwa ripoti za wataalamu sio halisi ama usahihi wake unatiliwa mashaka, la hasha. Ninachosisitiza ni uwezo wa kiongozi kuwafahamu watu wake kwa utashi wake binafsi.

Tanzania kama nchi imekuwa mhanga wa sera za namna hii (sera za jumla jumla). Wataalamu wanapewa pesa kufanya utafiti na ripoti zao mara nyingi huchambua mambo kwa jumla jumla. Ujumla huu unaweza kusaidia kujua ni eneo lipi la kuanzia kulifanyia kazi kwa reja reja. Hatua inayofuata ni kiongozi kushuka chini ngazi ya kuwafahamu watu wake kwa ureja reja (specific intervention).

Sababu nyingine kwa nini Tanzania imekuwa mhanga wa sera za jumla jumla ni kwa sababu ya kuyachukulia mambo kwa ujumla wake tangu awali. Athari ya sera hizi ni kutokuwa na kasi kubwa ya mabadiliko kwa kuwa mbinu ya kuleta mabadiliko huwa ile ya jumla jumla badala ya reja reja (specific transformation) kwa kuwa taarifa za awali huletwa jumla jumla na viongozi hupata uvivu wa kumeng’enya taarifa ziwe reja reja (specific issues)  


Kasi kubwa ya mabadiliko itakuwepo endapo kila kiongozi atawafahamu watu wake kwa undani na kushambulia kiini cha matatizo yao kwa mbinu ya urejereja (specific strategy of problem solving). Kwa mfumo wa viongozi tulionao ni muhimu kufahamu jambo moja moja kwa kina na kuepuka kuchukulia mambo kwa jumla jumla. Mtazamo huu utabadilisha kasi ya mabadiliko yetu kwa kuwa uwezo wa viongozi utaongezeka kwa kuwa kila kiongozi atakuwa anawafahamu watu wake kwa undani. 

No comments:

Post a Comment