Thursday, December 9, 2010

Baraza Jipya la Mawaziri ni Changamoto Mpya kwa Vijana wa Tanzania

Baraza jipya lililotangazwa hiivi punde na Mhe. Rais Jakaya Kikwete limeshuhudiwa kutolewa kwa idara ya vijana kutoka kwa iliyokuwa Wizara ya kazi, ajira na maendeleo ya vijana huku idara hiyo ikipelekwa katika wizara ya Habari, Michezo na Vijana.

Ukiangalia utofauti wa jina unaweza usipate mantiki ya kwa nini hapo awali wizara iliyoshughulikia mambo ya vijana ilipewa jina la “maendeleo ya vijana” na sasa katika wizara mpya kupewa jina “vijana” pekee. Swali la kujiuliza hapa ni kwamba je wizara hiyo ya zamani ilishindwa kuleta maendeleo ya vijana? Na kama lengo katika miaka mitano iliyopita ilkuwa ni kuleta maendeleo ya vijana je idara ya vijana katika iliyokuwa wizara ya maendeleo ya vijana je ilifanikiwa kufanya kazi kwa ufanisi kuwaletea vijana maendeleo kama ilivyojiita kuwa wizara ya maendelo ya vijana?

Majibu haya ya maswali mawili hapo juu anayo Mhe. Rais aliyefanya mageuzi na kuunda wizara nyingine itakayoshughulikia mambo ya vijana 2010-2015! Je suala ni kupeana ulaji au kuleta maendeleo kwa vijana hoja hii tutaipima miaka mitano ijayo itakapoisha. Mhe waziri uliyeteuliwa kazi kwako kuikanusha hoja hii kwa ufanisi wako ndani ya miaka mitano ama kuifanya kuwa kweli na kumuangusha bosi wako aliyekuteua.

Pamoja na changamoto nyingine zinazoikabili idara ya vijana ni uundwaji wa baraza huru la Taifa la Vijana. Kupigwa dana dana kwa idara hiyo ya vijana kunaweza kupelekea kukosekana kwa ufanisi hasa katika kusimamimia sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana. Hoja ya ufanisi wa idara ya vijana kusimamia uundwaji wa baraza la vijana ndani ya wizara mpya inaweza kuchelewesha mchakato huo.

Hapa vijana na wanaharakati tunapaswa kuwa makini kutoa msukumo na shinikizo ya hoja ya uharakishwaji na uwepo wa baraza huru la vijana ianze mapema. La sivyo madai yetu ya ongezeko la ajira kwa vijana hayawezi kufanyiwa kazi ipasavyo na idara hiyo endapo hatutakuwa na chombo chetu mathubuti cha kusimamania ajenda za vijana hapa nchi kama ilivyokuwa kwa nchi za jirani kama Uganda, Botswana na kwingineko.

Waziri husika uliyeteuliwa na Mhe. Rais kushika wadhifa katika wizara inayoshughulikia mambo ya vijana, nakuomba urejee ahadi ya Mtangulizi wako Mhe. Athuman Juma Kapuya aliyoitoa katika maadhimisho ya siku ya vijana kimataifa (IYD)tarehe 12 Agosti 2010 katika ukumbi wa Apeadu (United Nations Compound-Kinondoni) kuwa wizara ya vijana ipo tayari kusimamia uundwaji wa baraza huru la vijana la Taifa.Na baadaye Waziri mstaafu Kapuya kufungua mwaka wa kimataifa wa vijana (International Youth Year-IYY) ambapo Mpango kazi wa IYY uliundwa na vijana na kuwa na kipaumbele cha kwanza kinachotaka Vijana na Serikali kushirikiana kuunda Baraza Huru la Vijana la Taifa.

Mhe. Waziri mpya wa vijana unajukumu la kwanza kuhakikisha tunakuwa na baraza hili mapema kabla ya Januari 2012, pamoja na kuwa utakuwa na kazi ya kusimamia Habari na Michezo hili lisiwe kisingizio. Vijana chonde chonde tusichoke kukomalia suala la uanzishwaji wa Baraza Huru la Vijana,bila kujali utofauti wa itikadi za rangi, kabila na siasa.Miaka zaidi ya 13 imepita bila kuwa na baraza hili tangu vuguvugu za harakati hizi zianze; pamoja na ahadi ya sera ya maendeleo ya vijana isiyotekelezeka kudai kuwa serikali itasimamia uundwaji wake bila mafanikio kwa muda wa miaka yote hii. Sasa tumechoshwa na ahadi za sera isiyotekelezeka tunataka mtu shupavu, muadilivu na mchapa kazi kama alivyosema Mhe. Rais ambaye ndiye bosi wako kutoa msukumo maalumu wa uwepo wa Baraza, sisi vijana tunaamni mtu huyo mwenye sifa ilizosema Mhe.Rais ni wewe Mhe. Waziri mpya uliyeteuliwa hivi punde.